Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, taarifa nambari 3 ya Kamati ya Maadhimisho ya Kupaa Damu ya Imam Mujahid Shahidi, Ayatullah al-Udhma Khamenei (qaddasallahu nafsahu-z-zakiyyah), imechapishwa.
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
«مِنَ الْمُؤْمِنِینَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَیْهِ فَمِنْهُم مَّن قَضَی نَحْبَهُ وَمِنْهُم مَّن یَنتَظِرُ وَمَا بَدَّلُوا تَبْدِیلًا»
“Miongoni mwa Waumini wapo wanaume waliotimiza kwa ukweli ahadi waliyoahidi kwa Mwenyezi Mungu; miongoni mwao wapo waliotimiza muda wao, na miongoni mwao wapo wanaongoja, wala hawakubadilisha chochote.”
Kufuatia kupaa kwa damu ya Marjii Mkuu wa ulimwengu wa Kishia, Kiongozi mwenye hekima wa Mapinduzi ya Kiislamu na mbeba bendera wa kambi ya haki na Muqawama, Imam Mujahid Shahidi, Ayatullah al-Udhma Sayyid Ali Husseini Khamenei (qaddasallahu nafsahu-z-zakiyyah), ulimwengu wa Kiislamu umeketi katika maombolezo ya kumpoteza mtu mkubwa ambaye alitumia maisha yake yote yenye baraka katika kuinua neno la haki, kuutetea Uislamu, kuwahudumia watu na kuuongoza Umma wa Kiislamu.
Kiongozi huyo shahidi, kwa imani thabiti, jihadi ya ikhlasi, subira imara na utambuzi wa kimungu, daima aliiweka juu bendera ya uhuru wa Iran mpendwa na mwongozo pamoja na heshima ya Umma wa Kiislamu. Jina na kumbukumbu za mtu huyo wa kipekee wa zama zake zitabaki milele katika historia ya Iran pendwa, ulimwengu wa Kiislamu na katika nyoyo za watu huru duniani.
Kamati ya Maadhimisho ya Kupaa kwa Damu ya Imam Mujahid Shahidi, Ayatullah al-Udhma Khamenei (a‘la-llahu maqamahu-sh-sharif), huku ikitoa pole kwa Hadrat Waliyul-Asr (a.f), Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi, Ayatullah Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei, pamoja na mataifa yote huru na wapenda njia ya haki, inatoa shukrani na pongezi zake za dhati kwa ushiriki mkubwa na wa uaminifu wa watu wa Iran na wapenda Uislamu na Mapinduzi kutoka kila mahali.
Kwa kufuatia taarifa zilizotangulia za kamati hii, na kwa kuzingatia mipango iliyofanywa, wananchi wote waheshimiwa na waombolezaji wanataarifiwa kwamba; sherehe za kuaga, kusindikiza na kuzika mwili mtukufu wa Imam huyo Mujahid Shahidi pamoja na baadhi ya wanafamilia wake, yaani mashahidi watukufu Dkt. Misbah al-Huda Baqeri-Kani, Sayyida Bushra Husseini Khamenei, Zahra Haddad-Adel na Zahra Mohammadi Golpayegani (Ridwanullahi ‘alayhim ajma‘in), zitafanyika kama ifuatavyo:
Siku za Jumamosi tarehe 13 na Jumapili tarehe 14 Tir 1405 Shamsia, zinazolingana na tarehe 19 na 20 Muharram: Sherehe ya kuaga mwili mtukufu katika Musalla wa Imam Khomeini (q.s.) mjini Tehran.
Siku ya Jumatatu tarehe 15 Tir 1405 Shamsia, inayolingana na tarehe 21 Muharram: Sherehe ya mazishi na maandamano ya kusindikiza mwili mjini Tehran.
Siku ya Jumanne tarehe 16 Tir 1405 Shamsia, inayolingana na tarehe 22 Muharram: Sherehe ya mazishi na maandamano ya kusindikiza mwili katika mji mtakatifu wa Qom.
Siku ya Alhamisi tarehe 18 Tir 1405 Shamsia, inayolingana na tarehe 24 Muharram na usiku wa shahada ya Imam Sajjad (a.s.): Sherehe ya mazishi na maandamano ya kusindikiza mwili katika Mashhad Tukufu na kuzikwa katika Haram Tukufu ya Imam Ridha (as).
Wananchi wote waheshimiwa na wapendwa, watu huru duniani, wapenzi wa madrasa ya Uislamu na marafiki wa Iran wanaalikwa kushiriki katika sherehe hizi adhimu ili kumsindikiza kiongozi huyo shahidi katika safari yake ya mwisho.
Mwisho, huku tukitoa shukrani kwa maandalizi na mipango mikubwa iliyofanywa na taasisi husika na makundi ya wananchi kwa ajili ya kufanikisha tukio hili, tunasisitiza kwamba; jukumu kuu katika kuendesha sherehe hizi litabebwa na wananchi waheshimiwa na wenye kuwa daima mstari wa mbele, kama wamiliki wa kweli wa maombolezo haya, na kwamba kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, tukio hili litakuwa na sura adhimu na ya kipekee ya ushiriki wa wananchi.
Maelezo zaidi ya sherehe hizi yatatangazwa baadaye kwa umma.
Ofisi ya Kuhifadhi na Kuchapisha Athari za Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu
23 Khordad 1405 Shamsia/ June 14 2026
Maoni yako